Search Search
Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *

[KANUNI]

INDEX TO SUBSIDIARY LEGISLATION

    KANUNI

        Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa

KANUNI

KANUNI ZA BAHATI NASIBU YA TAIFA

    Fungu

Mpango wa Mafungu Mbali Mbali

SEHEMU YA I
UTANGULIZI

    1.    Jina na mwanzo.

    2.    Tafsiri.

SEHEMU YA II
BAHATI NASIBU YA KAWAIDA

    3.    Kuendesha Bahati Nasibu za kawaida.

    4.    Wakati wa kucheza.

    5.    Idadi ya tikiti zitakazotolewa.

    6.    Zawadi za Bahati Nasibu za kawaida.

SEHEMU YA III
BAHATI NASIBU MAALUM

    7.    Bahati Nasibu Maalum.

    8.    Tikiti zita chanishwa kwa kila Bahati Nasibu Maalum.

    9.    Zawadi za Bahati Nasibu Maalum.

SEHEMU YA IV
TIKITI ZA BAHATI NASIBU

    10.    Bei ya tikiti.

    11.    Tikiti kupewa nambari zinazofuatana.

    12.    Tikiti zitatolewa katika vijitabu.

    13.    Yaliyomo ndani ya tikiti.

SEHEMU YA V
UUZAJI WA TIKITI ZA BAHATI NASIBU

    14.    Uteuzi wa Maajenti wauzaji.

    15.    Barua ya kuteuliwa.

    16.    Dhamana.

    17.    Utanguo Maajenti Uuzaji.

    18.    Ugawaji wa tikiti kwa maajenti wauzaji.

    19.    Tarehe za kwanza kuuza tikiti.

    20.    Tarehe za kufunga kuuza wa tikiti.

    21.    Uuzaji wa tikiti utakoma tarehe ya mwisho.

    22.    Wajibu wa kurejesha tikiti zote zilizouzwa pamoja na vishina siku ya mwisho.

    23.    Wajibu wa kulipa fedha taslimu kutokana na tikiti zote zilizouzwa.

    24.    Maajenti wadogo.

    25.    Jina la mnunuzi kuandikwa katika kishina cha tikiti.

    26.    Tikiti haitanunuliwa na zaidi ya mtu mmoja.

    27.    Namna ya kutunza vitabu vya hesabu.

    28.    Wizi wa tikiti.

SEHEMU YA VI
MICHEZO

    29.    Mahali pa kuchezesha mchezo.

    30.    Kamati ya kusimamia mchezo.

    31.    Kuahirisha mchezo.

    32.    Utaratibu.

    33.    Ukaguzi wa mashine.

    34.    Taksiri itokeapo wakati wa mchezo.

    35.    Tikiti zilizouzwa tu zishiriki katika kuchagua zawadi tatu za kwanza.

    36.    Tikiti inaposhinda zaidi ya zawadi moja.

SEHEMU YA VII
MADAI YA ULIPAJI WA ZAWADI

    37.    Tafsiri.

    38.    Wenye mamlaka ya kulipa.

    39.    Madai ya zawadi.

    40.    Tikiti zilizopotea.

    41.    Zawadi zisizodaiwa baada ya miezi sita.

    42.    Zawadi za wauzaji.

SEHEMU YA VIII
MIPANGO YA USALAMA

    43.    Tikiti zote zilizouzwa kuwekwa mahali pa usalama.

    44.    Kufungua vifurushi vya tikiti zisizouzwa.

    45.    Tikiti zisizouzwa zinazofika baada ya siku ya mchezo.

    46.    Kuharibu tikiti zisizouzwa.

SEHEMU YA IX
MAKOSA

    47.    Kushindwa kurejeshwa tikiti zisizouzwa.

    48.    Habari ya udanganyifu.

    49.    Kuharibu kifurushi chenye tikiti zisizouzwa.

    50.    Adhabu.

NYONGEZA

KANUNI
KANUNI ZA BAHATI NASIBU YA TAIFA

(Chini ya kifungu cha 20)

[1 Januari, 1978]

T.S. Na. 48 ya 1979

SEHEMU YA I
UTANGULIZI

1.    Jina la mwanzo

    Kanuni hizi zitaitwa Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa.

2.    Tafsiri

    Katika Kanuni hizi, mpaka iwapo maana nyingine itahitajika–

    "Bahati Nasibu" maana yake ni Bahati Nasibu ya Taifa;

    "Bahati Nasibu Maalum" maana yake ni Bahati Nasibu isiyo ya kawaida ambayo huendeshwa na kuchezeshwa na Mkurugenzi kwa kibali cha Bodi ili kuadhimisha sikukuu yoyote ile ya Taifa au siku ya mapumziko;

    "Bahati Nasibu ya Kawaida" maana yake ni Bahati Nasibu ambayo inaendeshwa na kuchezeshwa mara moja kila mwezi kwa kufuatana na vifungu vya Kanuni hizi;

    "Kamati" maana yake ni Kamati ya kusimammia Uchezeshaji ambayo imeteuliwa na Bodi chini ya Kifungu cha 30 cha Kanuni hizi;

    "Mamlaka ya ulipaji" maana yake ni mtu ambaye ameruhusiwa na Kanuni hizi kulipa zawadi kwa wenye tikiti zilizoshinda;

    "Sheria" maana yake ni Sheria ya Bahati Nasibu ya Taifa *;

    "tarehe ya mwanzo" maana yake ni tarehe ambayo uuzaji wa tikiti za Bahati Nasibu kwa ajili ya mchezo wowote ule wa Bahati Nasibu utaanza;

    "tarehe ya mwisho" maana yake ni tarehe ambayo uuzaji wote wa tikiti za Bahati Nasibu kwa ajili ya mchezo wowote ule wa Bahati Nasibu utakoma;

    "tikiti" maana yake tikiti ya Bahati Nasibu;

    "Utaratibu" maana yake ni tangazo ambalo limetolewa katika Gazeti la Serikali ambamo kuna habari kamili ambazo zinahitaji kutangazwa na Bodi kwa kufuatana na ibara ya (a) ya kifungu 7 cha Sheria ya Bahati Nasibu.

SEHEMU YA II
BAHATI NASIBU YA KAWAIDA

3.    Kuendesha Bahati Nasibu za kawaida

    Bodi itaendesha bahati nasibu ya kawaida mara moja kila mwezi.

4.    Wakati wa kucheza

    Mchezo wowote ule wa kawaida ambao utaendeshwa kila mwezi, kwa kufuata vifungu vya sehemu ya VI, utaendeshwa kati ya siku ya kwanza na ya ishirini na tano ya mwezi unaofuata, kama Mkurugenzi atakavyoamua.

5.    Idadi ya tikiti zitakazotolewa

    Mkurugenzi atachapisha tikiti kama itakavyoagizwa na Bodi kwa ajili ya kila mchezo wa Bahati Nasibu ya kawaida.

6.    Zawadi za Bahati Nasibu za kawaida

    Kutakuweko na zawadi zifuatazo katika kila mchezo wa kawaida wa Bahati ambazo zitatangazwa katika Gazeti la serikali na magazeti mengine kama itakavyoamriwa na Bodi:

    (a)    Zawadi ya Kwanza;

    (b)    Zawadi ya Pili;

    (c)    Zawadi ya Tatu;

    (d)    Zawadi ya Nne, zawadi mbili;

    (e)    Zawadi ya Tano, zawadi ishirini;

    (f)    Zawadi ya Sita, zawadi mia moja hamsini;

    (g)    Zawadi ya Saba, zawadi elfu moja na mia;

    (h)    Zawadi ya Nane, zawadi kumi na tano elfu.

SEHEMU YA III
BAHATI NASIBU MAALUM

7.    Bahati Nasibu Maalum

    (1) Pamoja na Bahati Nasibu za Kawaida Mkurugenzi anaweza kwa kibali cha Bodi, kuendesha Bahati Nasibu Maalum kuadhimisha sikukuu yoyote ya taifa au siku ya mapumziko.

    (2) Mchezo wa bahati Nasibu Maalum, kwa kufuatana na vifungu vya sehemu ya VI, utachezwa siku ambayo Mkurugenzi ataiweka katika utaratibu.

8.    Tikiti zitachapishwa kwa kila Bahati Nasibu Maalum

    Bodi itachapisha tikiti kwa idadi itakavyoamua, kwa ajili ya kila Bahati Nasibu Maalum.

9.    Zawadi za Bahati Nasibu Maalum

    (1) Bodi itaweka zawadi, katika kila mchezo wa Bahati Nasibu Maalum, ambazo zitatangazwa katika Gazeti la Serikali pamoja na magazeti mengine kama itakavyoamriwa na Bodi.

    (2) Bodi yaweza kubadili kima cha zawadi, kwa kutangaza katika Gazeti la serikali pamoja na magazeti mengine kama itakavyoonelea sawa katika kila Bahati Nasibu Maalum.

SEHEMU YA IV
TIKITI ZA BAHATI NASIBU

10.    Bei ya tikiti

    Bei ya kila tikiti kwa ajili ya bahati nasibu ya kawaida itawekwa na Bodi.

11.    Tikiti kupewa nambari zinazofuatana

    Tikiti zote zilizochapishwa kwa ajili ya bahati nasibu zitapewa nambari zinazofuatana kutoka nambari moja.

12.    Tikiti zitatolewa katika vijitabu

    (1) Tikiti zitatolewa katika vijitabu ndani yake zikiwamo tikiti ambazo idadi yake itakuwa kama itakavyoamua Bodi na kila tikiti itakuwa na kishina ambamo nambari itakayochapwa italingana na nambari ambayo itachapwa juu ya tikiti yenyewe ambayo pia iwe na nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuandika juu yake jina na anwani ya aliyenunua tikiti na jina na anwani ya muuzaji.

    (2) Jalada la kila kijitabu litakuwa limechapwa nambari ya kwanza na ya mwisho ya tikiti zilizomo katika kijitabu hicho na itakuwepo nafasi pia kwa ajili ya kuandika juu yake jina la muuzaji au mtu ambaye ameruhusiwa kuuza tikiti ambaye amepewa kijitabu hicho ili tikiti zilizomo ziuzwe.

13.    Yaliyomo ndani ya tikiti

    (1) Juu ya kila tikiti kutachapwa:

    (a)    nambari inayofuatana;

    (b)    bei ya tikiti;

{mprestriction ids="1,2,3"}

    (c)    tarehe ya mchezo;

    (d)    jambo jingine lolote ambalo Bodi itaona linafaa.

    (2) Bodi itachapisha nyuma ya kila tikiti maelezo yanayohusu:

    (a)    tarehe ya kuanza kuuza tikiti;

    (b)    tarehe ya mwisho wa kuuza tikiti;

    (c)    namna ya kudai zawadi; na

    (d)    jambo jingine lolote lile ambalo Bodi itaona linafaa.

SEHEMU YA V
UUZAJI WA TIKITI ZA BAHATI NASIBU

14.    Uteuzi wa Maajenti wauzaji

    (1) Tikiti zinaweza kuuzwa na watu ambao wameruhusiwa na Bodi kwa niaba yao au maajenti ambao wameteuliwa na Bodi, au na Mkurugenzi kwa niaba ya Bodi.

    (2) Ajenti wa uuzaji anaweza akamteua ajenti mmoja au zaidi kuuza tikiti za bahati nasibu kwa niaba yake kwa mapatano na masharti ambayo wanaweza wakakubaliana wao wenyewe.

15.    Barua ya kuteuliwa

    Wakati ajenti anapoteuliwa, Mkurugenzi atampa ajenti huyo barua ya kuteuliwa yenye umbile kama inavyoonyeshwa katika Jedwali iliyomo katika Kanuni hizi.

16.    Dhamana

    Mtu hatateuliwa kuwa ajenti wa uuzaji mpaka awe amekwisha mpa Mkurugenzi dhamana ya kiasi ambacho Mkurugenzi ataona kinafaa. Kila dhamana ya namna hiyo itakuwa katika umbile kama inavyoonyeshwa katika Jedwali iliyomo katika Kanuni hizi na itatiwa sahihi na ajenti wa uuzaji na wadhamini wawili ambao watakaokubaliwa na Bodi, au Mkurugenzi kwa niaba ya Bodi.

17.    Utanguo Maajenti Uuzaji

    Bodi inaweza kutengua kuteuliwa kwa ajenti muuzaji kwa kumpa notisi ya mwezi mmoja kwa maandishi, iwapo itaridhika kwamba ajenti hatimizi wajibu wake kama ajenti wa uuzaji au amekwenda kinyume cha Kifungu chochote kile cha Sheria au kanuni hizi au sehemu yoyote ile ya mapatano yaliyomo katika barua yake ya kumteua, au kwa sababu nyingine yoyote ile.

18.    Ugawaji wa tikiti kwa maajenti wauzaji

    Kila ajenti atapewa kiasi fulani cha tikiti kama atakavyoomba au kiasi cha tikiti ambacho Mkurugenzi ataona kinafaa, siyo chini ya siku kumi na kabla ya tarehe ya kuanza kuuza.

19.    Tarehe ya kuanza kuuza tikiti

    (1) Tarehe ya mwanzo ya bahati nasibu yoyote ya kawaida itakuwa ni siku ya kwanza ya mwezi ule uliotangulia mwezi wa mchezo.

    (2) Tarehe ya mwanzo ya bahati nasibu maalum itakuwa kama Bodi itakavyoamua.

20.    Tarehe za kufunga kuuza tikiti

    (1) Tarehe ya kufunga bahati nasibu itakuwa kama itakavyowekwa na Mkurugenzi.

    (2) Mkurugenzi aweza kuchagua tarehe tofauti za kufunga bahati nasibu kwa mahali tofauti.

    (3) Tarehe za mwisho zitaonyeshwa katika utaratibu.

21.    Uuzaji wa tikiti utakoma tarehe ya mwisho

    Hakuna mtu aliyeidhinishwa kuuza tikiti katika sehemu fulani kwa niaba ya Bodi au kama ajenti mdogo, ataendelea kuuza tikiti yoyote ya bahati nasibu baada ya tarehe ya mwisho iliyowekwa kwa ajili sehemu ile kwa ajili ya bahati nasibu yoyote ile.

22.    Wajibu wa kurejesha tikiti zote zilizouzwa pamoja na vishina siku ya mwisho

    (1) Kila ajenti au mtu mwingine ambaye ameruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yao atahakikisha kwamba siku mbili baada ya tarehe ya mwisho atamrudishia Mkurugenzi vishina vyotwe vya tikiti ambazo ameziuza na tikiti zote zisizouzwa alizonazo ambazo ni za bahati nasibu ambayo inahusiana na tarehe hiyo ya mwisho pamoja na hesabu kamili ya tikiti ambazo zilizouzwa na zisizouzwa kwa namna ambayo Bodi itaelekeza. Tikiti zisizouzwa zitakatwa kidogo kona ya juu kulia na ajenti kwa tahadhari kabla hazijarudishwa kwa Mkurugenzi.

    (2) Iwapo ajenti au mtu yeyote aliyeruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yao anaishi nje ya Dar es Salaam, atahakikisha kwamba siku mbili baada ya tarehe ya mwisho, anatuma vishina vyote vya tikiti ambazo ameziuza na tikiti zote zisizouzwa kwa ajili ya bahati nasibu ambayo inahusiana na tarehe hiyo ya mwisho kwa njia ya rejesta katika posta pamoja na orodha na hesabu ya tikiti zilizouzwa na zisizouzwa kwa namna ambayo Mkurugenzi ataelekeza. Tikiti zisizouzwa zitakatwa na ajenti kwa tahadhari kabla hazijatumwa kama ilivyoelezwa katika kifungu 22(1).

    (3) Nakala moja ya orodha ya tikiti zilizouzwa na zisizouzwa itapelekwa kwa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya kwa kuhifadhiwa na nyingine itatumwa pekee katika rejesta kwa Mkurugenzi wa bahati Nasibu ya Taifa.

    (4) Nakala ya orodha ya tikiti zilizouzwa na zisizouzwa itachukuliwa kuwa kithibitisho cha kuonyesha tikiti zilizouzwa na zile zisizouzwa.

23.    Wajibu wa kulipa fedha taslimu kuto-kana na tikiti zote zilizouzwa

    Kila ajenti au mtu mwingine yeyote ambaye ameruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yake atahakikisha kwamba kwa muda wa siku saba baada ya tarehe ya mwisho, atarejesha kwa Mkurugenzi kiasi cha fedha inayolingana na thamani ya tikiti zilizouzwa:

    Isipokuwa ajenti atakuwa na haki ya kuchukua kiasi fulani kama ni ujira wake; kiasi ambacho kinalingana na asilimia kumi na tano ya jumla ya fedha yote, au kama itakavyoamuliwa na Bodi.

24.    Maajenti wadogo

    Iwapo ajenti amemwajiri ajenti mwingine kuuza tikiti kwa niaba ya ajenti huyo, itakuwa ni wajibu wa ajenti mwenyewe kuchukua mapema vishina vyote vya tikiti zilizouzwa kutoka kwa ajenti huyo, na tikiti zote zisizouzwa alizonazo ajenti huyo ili kumwezesha ajenti mwenyewe kutimiza masharti ya ibara ya 22.

25.    Jina la mnunuzi kuandikwa katika kishina cha tikiti

    Itakuwa ni wajibu wa mtu anayeuza tikiti za bahati nasibu kwa niaba ya Bodi au kama ajenti mdogo kuhakikisha kwamba majina kamili na anuani ya mnunuzaji vinaonekana wazi wazi katika kishina.

26.    Tikiti haitanunuliwa na zaidi ya mtu mmoja

    (1) Tikiti haitanunuliwa na, au kuwa ni mali ya, zaidi ya mtu mmoja.

    (2) Iwapo kishina au tikiti yoyote ile imeandikwa majina ya watu wawili au zaidi kama ndio wanunuzi wa tikiti hiyo, mtu ambaye jina lake ni la kwanza katika kishina atakuwa ndiye mwenye tikiti hiyo kwa mujibu wa Sehemu ya VII na kufuatana na vifungu vya sehemu hiyo.

27.    Namna ya kutunza vitabu vya hesabu

    (1) Bodi itaweka kitabu maalum kwa ajili ya kila mtu aliyeruhusiwa nayo kuuza tikiti za bahati nasibu.

    (2) Katika kila kitabu kutakuwa na haya yafuatayo kuhusu kila habati nasibu:

    (a)    nambari ya mchezo;

    (b)    tikiti zilizopewa muuzaji;

    (c)    nambari ya tikiti hizo ambazo zinafuatana;

    (d)    thamani ya tikiti;

    (e)    kiasi cha fedha kilichopokelewa;

    (f)    nambari za hati za kutolea vitabu na tarehe zilizotolewa;

    (g)    hesabu ya tikiti zilizouzwa;

    (h)    hesabu ya tikiti zisizouzwa ambazo zimerudishwa na tarehe zilipopokelewa;

    (i)    nambari zinazofuatana, za tikiti ambazo zimerudishwa.

28.    Wizi wa tikiti

    Iwapo tikiti yoyote ile ambayo imetolewa kwa ajenti au mtu mwingine aliyeruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yao imeibiwa, ajenti au mtu huyo mwingine ataripoti mara moja wizi huo polisi na kumfahamisha Mkurugenzi juu ya wizi huo na iwapo tikiti hiyo itapatikana kabla ya tarehe ya mwisho ya bahati nasibu ambayo inahusiana na tikiti hiyo, Mkurugenzi atafahamishwa mara moja juu ya kupatikana kwa tikiti zao na majina yao yataorodheshwa na kuchapishwa katika karatasi ambayo itasambazwa kwa Maafisa hazina wa Wilaya na kwa Maajenti wote.

SEHEMU YA VI
MICHEZO

29.    Mahali pa kuchezesha mchezo

    Mchezo wa bahati nasibu utafanyika mahala na wakati ambao Mkurugenzi atateua.

30.    Kamati ya kusimamia mchezo

    (1) Mkurugenzi, kwa kibali cha Bodi, atawateua watu sita kuunda kamati itakayojulikana kama Kamati ya usimamizi wa Mchezo.

    (2) Kila mchezo utafanyika mbele ya Wajumbe watatu wa Kamati hiyo.

    (3) Mchezo ukiishamalizika Wajumbe wa Kamati waliopo wakiridhika kama mchezo uliendeshwa vema na kufuatana na Kanuni hizi watatoa cheti cha uthibitisho kuelezea matokeo ya mchezo.

    (4) Hati yoyote ya uthibitisho ambayo inatolewa kufuatana na ibara ya (3) itatiwa sahihi na wajumbe wa Kamati waliohudhuria katika mchezo.

31.    Kuahirisha mchezo

    (1) Mkurugenzi anaweza kuahirisha mchezo au michezo ya bahati nasibu yoyote au kwa ajili ya zawadi au zawadi zozote zile ikiwa akiona kwamba ni lazima au ni vizuri kufanya hivyo.

    (2) Iwapo mchezo umeahirishwa, tangazo kuelezea jambo hilo litatolewa katika gazeti au magazeti kama Mkurugenzi atakavyoamua.

32.    Utaratibu

    (1) Kila mchezo utaendeshwa kwa kutumia utaratibu unaotumika sasa wa kutumia pipa (drum) mpaka hapo mabadiliko yatakapofanywa na kupata mashine za kawaida kama inavyoelezwa katika ibara ya (3).

    (2) Wakati ambapo pipa litatumika utaratibu unaofuata utatumika ikiwa tikiti zilizochapwa ni tikiti 150,000. Utaratibu utageuzwa kufuatia mabadiliko ya namba za tikiti zitakazochapishwa:

    (i)    Kufuatana na kanuni hizi, kabla ya mchezo wowote haujachezeshwa, Mkurugenzi atahakikisha kuwa kumetengenezwa vikaratasi 150,000 ambavyo vimechapishwa namba, kikaratasi cha kwanza kikiwa na namba 1 na cha mwisho kikiwa na namba 150,000.

    (ii)    Mchezo wowote utakaochezwa kutumia pipa utafuta utaratibu huu:

        (a)    Kabla ya saa za mchezo kila kikaratasi, kati ya hivyo vilivyotayarishwa na namba, kitakunjwa kwa njia atakayoiona Mkurugenzi kuwa sawa.

        (b)    Wakati wa kuanza mchezo vikaratasi vyote vilivyokunjwa vitatiwa ndani ya pipa.

        (c)    Ili kuchagua mshindi wa zawadi ya kwanza, papa litazungushwa mara kadhaa wa kadha ili kuhakikisha kuwa vikaratasi vimechanganyika vizuri, na baada ya piapa kusimama:

            (i)    Dirisha moja litafunguliwa, kikaratasi kimoja kitatolewa, na namba ya kikaratasi hicho itatangazwa kuwa ndiyo iliyoshinda.

            (ii)    Baadaye kikaratasi hicho kilicho na namba iliyoshinda kitakunjwa tena na kurudishwa ndani ya pipa kabla ya zawadi ifuatayo kutafutwa.

        (d)    Utaratibu ulioelezwa katika (c) utafuatwa kwa zawadi ya kwanza hadi ya tano.

        (e)    Katika kutafuta washindi wa zawadi ya sita, utaratibu ulioelezwa katika (c) utafuatwa na ikiwa:

            (i)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu nne au zaidi, tikiti zote zilizo na namba ambazo tarakimu zake nne za mwisho zafanana na tarakimu hizo zitatangazwa kuwa ni za ushindi.

            (ii)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu tatu, tikiti zote ambazo tarakimu zake nne za mwisho zafanana na tarakimu hizo zitatangazwa kuwa ni za ushindi.

            (iii)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina tarakimu zisizofika nne zawadi hiyo itachezeshwa tena.

        (f)    Katika kutafuta washindi wa zawadi ya saba utaratibu ulioelezwa katika (c) utafuatwa na ikiwa:

            (i)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu tatu au zaidi, tikiti zote zilizo na namba ambazo tarakimu zake tatu za mwisho zafanana na tarakimu hizo zitatangazwa kuwa ni za ushindi.

            (ii)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu mbili, tikiti zote ambazo tarakimu zake tatu za mwisho zafanana na tarakimu hizo zitatangazwa kuwa ni za ushindi.

            (iii)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu mbili, zawadi hiyo itachezeshwa tena.

        (g)    Katika kutafuta washindi wa zawadi ya nane utaratibu ulioelezwa katika (c) utafuatwa na ikiwa:

            (i)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu mbili au zaidi, tikiti zote ambazo tarakimu ya mwisho inafanana na tarakimu ya mwisho ya namba ya tikiti iliyochaguliwa, zitakuwa za ushindi.

            (ii)    Kama kikaratasi kilichochaguliwa kina namba iliyo na tarakimu moja zawadi hiyo itachezeshwa tena.

    (3) Wakati ambapo mashine za kawaida zinatumika na tikiti 150,000 zimechapishwa uataratibu ufuatao utafuatwa:

    (a)    Mashine sita zitawekwa katika mstari mmoja na kupewa alama kuanzia kushoto kuelekea kulia A, B, C, D, E na F.

    (b)    Mashine A itarekebishwa hivi kwamba itaweza kuonyesha 0 na 1.

    (c)    Mashine B itarekebishwa ili iweze kuonyesha tarakimu yoyote kuanzia 0 hadi 4.

    (d)    Mashine zingine zilizobakia zitarekebishwa ili ziweze kuonyesha tarakimu yoyote kuanzia 0 hadi 9.

    (e)    Kwa ajili ya mchezo wa zawadi ya kwanza mashine zote sita zitatumika na nambari itakayotokea badala ya kuweka tarakimu zote pamoja zitakazoonekana kwenye mashine A, B, C, D, E na F kwa mpango wa namna hii itakuwa ndiyo nambari iliyoshinda; na iwapo nambari hiyo ni 000000 nambari iliyoshindwa itakuwa ni 150,000.

    (f)    Kwa ajili ya mchezo wa zawadi ya pili, ya tatu hadi ya tano mpango kama huu ulioelezwa katika kifungu (e) utafuatwa kwa ajili ya kila zawadi; yaani kwa ajili ya kila zawadi, nambari itakayotokea baada ya kuweka tarakimu zitakazoonekana juu ya mashine A, B, C, D, E na F kwa mpango wa namna hii itakuwa ndiyo nambari iliyoshinda zawadi katika mchezo huo, iwapo nambari iliyotokea itakuwa ni 000000 nambari iliyoshinda itakuwa 150,000.

    (g)    Kwa ajili ya mchezo wa zawadi ya sita ni mashine D, na F tu ndizo zitakazotumika na tarakimu tatu za mwisho katika kila tikiti ambazo zitafuatana na tarakimu ambazo zitaonekana baada ya kuweka pamoja tarakimu zitakazoonekana katika mashine D, E na F kwa mpango huu itakuwa ndiyo tikiti iliyoshinda.

    (h)    Kwa ajili ya mchezo wa zawadi ya saba katika bahati nasibu ya kawaida ni mashine E na F tu ndizo zitakazotumika na kila tikiti yenye tarakimu mbili za mwisho ambazo zinalingana na zile zinazoonekana kwenye mashine kama ilivyo katika mpango huu itakuwa ndiyo tikiti iliyoshinda.

    (i)    Kwa ajili ya zawadi ya nane katika mchezo wa kawaida au zawadi ya sita katika mchezo maalum ni mashine F tu ndiyo itakayotumika na kila tikiti yenye tarakimu ya mwisho inayolingana na tarakimu inayoonekana katika mashine itakuwa ndiyo tikiti iliyoshinda.

    (j)    Utaratibu huu utageuka kulingana na namba ya tikiti zitakazochapishwa kwa kila mchezo.

33.    Ukaguzi wa mashine

    Kabla ya mchezo wa kutumia mashine yoyote haujaanza, mtu ambaye amechaguliwa na Mkurugenzi, atakagua mashine hiyo na mchezo hautachezwa kabla ya fundi huyo kuridhika kuwa mashine hiyo inafanya kazi sawa sawa.

34.    Taksiri itokeapo wakati wa mchezo

    Iwapo wakati wa mchezo wajumbe wa kamati ya kusimamia mchezo wameridhika kuwa mashine yoyote ina hitilafu au kwamba mashine yoyote haifanyi kazi sawa sawa wanaweza kuahirisha mchezo mpaka mashine hiyo imetengenezwa au imepatikana nyingine iliyo nzima.

35.    Tikiti zilizo-uzwa tu zishiriki katika kuchagua zawadi za kwanza

    (1) Iwapo nambari itakayochezwa kwa ajili ya zawadi yoyote ile kati ya zile zawadi tatu za kwanza ni nambari ya tikiti ambayo haikuuzwa, zawadi hiyo itachezeshwa tena mara moja.

    (2) Iwapo kuna mashaka yoyote kwamba tikiti yenye nambari ya ushindi, imeshinda au haikushinda mojawapo ya zawadi tatu za kwanza, na kama hakuna uhakika kwamba imeuzwa, mkurugenzi, anaweza akaamuru uchunguzi ufanywe na baada ya uchunguzi huo akiridhika kwamba tikiti hiyo haikuuzwa, mpango wa mchezo kuhusu zawadi hiyo utafanywa bila kukawia.

    (3) Mkurugenzi anaweza, kwa ajili ya uchunguzi wowote chini ya ibara ya (2) kuahirisha mchezo wa zawadi fulani kwa muda wowote ule ambao ataona unafaa.

36.    Tikiti inapo-shinda zaidi ya zawadi moja

    (1) Iwapo tikiti moja itashinda zawadi mbili au zaidi kati ya zile zawadi tatu za kwanza katika bahati nasibu yoyote ile, tikiti hiyo itatajwa kuwa mshindi wa zawadi iliyo ya juu zaidi kati ya hizo zawadi, na zingine zitachezwa tena mara moja.

    (2) Mshindi anaweza kulipwa zaidi ya zawadi moja ikiwa zawadi ya pili itakuwa ni mojawapo ya zile zawadi za kuhesabu tarakimu za mwisho.

SEHEMU YA VII
MADAI YA ULIPAJI WA ZAWADI

37.    Tafsiri

    Katika sehemu hii mpaka pawepo na haja ya maana nyingine–

    "mwenyewe" maana yake:

    (a)    Kuhusiana na tikiti ambayo imeshinda mojawapo ya zawadi tatu za kwanza, mtu ambaye jina lake linaonekana katika kishina kama ndiye mnunuzi wa tikiti, na pia inamaanisha–

        (i)    iwapo mtu ambaye jina lake linaonekana katika kishina amekufa, mrithi wake au mwangalizi wa mali zake;

        (ii)    kwa yule mtu ambaye jina lake limeonekana katika kishina lakini hana akili timamu, mtu ambaye ameteuliwa kuangalia mali zake chini ya Sheria ya ugonjwa wa Kichaa;

        (iii)    iwapo jina la mtu linaonekana katika kishina ni la mtu mwenye umri chini ya miaka kumi na mitano, baba yake, iwapo baba amekufa au hawezi kupatikana baada ya kumtafuta, mama ya mtoto huyo au, iwapo mama amekufa au hawezi kupatikana baada ya kumtafuta, mtu ambaye kwa maoni ya Mkurugenzi ndiye mlezi wa mshindi huyo;

        (iv)    iwapo mama yake mtoto amemnunulia tikiti mwanawe aliye chini ya miaka kumi na tano, mama yake, iwapo mama yake amekufa au hawezi kupatikana baba yake au, iwapo baba yake amekufa au hawezi kupatikana mtu ambaye kwa maoni ya Mkurugenzi ndiye mlezi wa mshindi huyo;

        (v)    iwapo mtu yule ambaye jina lake linaonekana katika kishina amempa tikiti hiyo mtu mwingine ubadilishaji huu wa tikiti hautakubaliwa au yule aliyepewa tikiti hiyo, hatakubaliwa kama ndiye mwenyewe mpaka atakapomridhisha Mkurugenzi juu ya ubadilishaji huo.

    (b)    Kuhusu tikiti ambayo imeshinda zawadi nyingine yoyote ile, mtu ambaye atakuwa anayo ile tikiti wakati wa kuionyesha ili kudai zawadi ndiye atakayepewa zawadi baada ya kupata uthibitisho kwamba ndiye mshindi.

38.    Wenye mamlaka ya kulipa

    (1) Kuhusu zawadi ya shilingi elfu moja na zaidi katika bahati nasibu ya kawaida na zawadi ya shilingi elfu moja na zaidi katika bahati nasibu maalum, mwenye mamlaka ya ulipaji atakuwa ni Mkurugenzi, au afisa wa cheo cha juu aliyeidhinishwa na Mkurugenzi kufanya hivyo.

    (2) Kuhusu zawadi zilizobakia, wenye mamlaka ya ulipaji watakuwa ni Maafisa wa fedha wa Idara ya Hazina Wilayani na Maajenti, au watu wowote wale ambao Mkurugenzi anaweza akawateua kama maafisa wa ulipaji.

39.    Madai ya zawadi

    (1) Mwenye tikiti iliyoshinda ataweza kulipwa zawadi ambayo tikiti hiyo imeshinda atakapoionyesha na kuitoa kwa mwenye mamlaka ya kufanya malipo na kuwaridhisha hao wenye kufanya malipo kwamba yeye ndiye hasa mwenye tikiti hiyo.

    (2) Wakati tikiti inapoonyeshwa na kutolewa kwa wenye mamlaka ya kufanya malipo, na zawadi ikilipwa kwa mwenye tikiti, mwenye mamlaka ya kufanya malipo atie alama au muhuri juu ya tikiti hiyo wenye maneno "imelipwa".

    (3) Iwapo wenye mamlaka ya kufanya malipo, lakini siyo Mkurugenzi atapewa tikiti ambayo:

    (i)    siyo kamili au imefanyiwa mabadiliko au imekwaruzwa kwaruzwa au imefutwa futwa;

    (ii)    kwa maoni ya mwenye mamlaka ya kufanya malipo ya kwamba tikiti isiyo halali mara moja atampa mwenye tikiti hiyo karatasi ya kuthibitisha kwamba ameipokea tikiti hiyo na kuituma tikiti hiyo mwenye mamlaka hiyo kwa Mkurugenzi wa bahati Nasibu kwa uamuzi wake chini ya kifungu 7(e) cha sheria iwapo zawadi hiyo ilipwe au hapana.

40.    Tikiti zilizopotea

    (1) Iwapo mtu yeyote anadai kwamba ndiyo mwenye tikiti ambayo imeshinda na ameipoteza:

    (a)    iwapo tikiti hiyo ndiyo iliyoshinda mojawapo ya zawadi tatu za kwanza, Mkurugenzi, kwa niaba ya Bodi atateua Kamati ya watu watatu kuchunguza madai ya mtu huyo kwa njia ambayo kamati itaona sawa na kutoa taarifa ya yale waliyoyaona kwa Mkurugenzi;

    (b)    iwapo tikiti hiyo imeshinda zawadi yoyote ile nyingine, mdai akakataa zawadi hiyo mpaka mdai huyo amridhishe Mkurugenzi kwamba tikiti hiyo aliuziwa yeye au kwamba yeye anaimiliki tikiti hiyo kwa njia ya halali.

    (2) Iwapo kamati iliyoteuliwa chini ya kifasili (a) cha fasili (1) itaona kwamba dai la mwenye kudai ni la haki basi Mkurugenzi atamlipa mwenye kudai inayopasa kwa kufuata masharti ya kulipa zawadi kama ambavyo Mkurugenzi huyo ataona inafaa, na kufanya mapumziko yasiyozidi sehemu moja ya kumi ya thamani ya zawadi hiyo kama itakavyoagizwa na Bodi kuwa ndio ada kwa ajili ya uchunguzi.

41.    Zawadi zisizodaiwa baada ya miezi sita

    Ikiwa zawadi yoyote ya tikiti iliyoshinda haikudaiwa baada ya muda wa miezi 6 tangu tarehe ya mchezo zawadi hiyo haitalipwa kwa tikiti hiyo iliyoshinda, na zawadi hiyo itaingizwa katika mfuko wa Bahati Nasibu ya Taifa.

42.    Zawadi za wauzaji

    (1) Iwapo tikiti iliyoshinda mojawapo ya zawadi zile tatu za kwanza ilitolewa kuuzwa na ajenti muuzaji:

    (a)    iwapo tikiti hiyo ilikuwa na ajenti, Mkurugenzi atamlipa ajenti huyo zawadi ya uuzaji ambayo ni sawa na asilimia tano ya zawadi ambayo tikiti hiyo imeshinda;

    (b)    iwapo tikiti hiyo iliuzwa na ajenti, Mkurugenzi atamlipa ajenti hivi–

        (i)    kwa ajenti mdogo, zawadi ya muuzaji ambayo ni sawa na asilimia tatu ya zawadi ambayo tikiti hiyo imeshinda; na

        (ii)    kwa ajenti mwenyewe zawadi ya muuzaji ambayo ni sawa na kiasi cha asilimia mbili ya zawadi ambayo tikiti hiyo imeshinda.

    (2) Iwapo tikiti hiyo ambayo imeshinda mojawapo ya zawadi tatu za kwanza iliuzwa na mtu ambaye aliruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yake, Mkurugenzi atamlipa mtu aliyeiuza tikiti hiyo zawadi ya muuzaji kiasi ambacho ni sawa na asilimia tano ya zawadi ambayo tikiti hiyo imeshinda.

SEHEMU YA VIII
MIPANGO YA USALAMA

43.    Tikiti zote zilizouzwa kuwekwa mahali pa usalama

    Siku inayotangulia tarehe ya mchezo wowote ule wa Bahati Nasibu, Mkurugenzi ataweka tikiti zote zisizouzwa ambazo zinahusiana na mchezo huo katika chumba imara au sanduku za kuhifadhi fedha ambamo yeye Mkurugenzi tu au mtu mwingine ambaye ameruhusiwa kwa maandishi anaweza kuingia.

44.    Kufungua vifurushi vya tikiti zisizouzwa

    Kila kifurushi chenye tikiti zisizouzwa ambazo zimetumwa na ajenti au mtu mwingine aliyeruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kitafunguliwa na Mkurugenzi tu au mtu mwingine aliyeruhusiwa na yeye mwenyewe.

45.    Tikiti zisizouzwa zinazofika baada ya siku ya mchezo

    Iwapo kifurushi chochote chenye tikiti zisizouzwa kitamfikia Mkurugenzi baada ya siku inayotangulia tarehe ya mchezo wa bahati Nasibu ambao unahusiana na tikiti hizo zisizouzwa, Mkurugenzi atakiweka kifurushi cha tikiti hizo zote zisizouzwa katika chumba cha usalama mara moja au katika sanduku la fedha kwa kufuatana na vifungu vya kanuni ya 43.

46.    Kuharibu tikiti zisizouzwa

    Iwapo mchezo unaohusiana na bahati nasibu fulani umechezeshwa, Mkurugenzi ataamuru kubatiliwa kwa tikiti zote zisizouzwa ambazo zinahusiana na mchezo huo bila kuchelewa, mbele yake yeye mwenyewe au mbele ya mtu mwingine yeyote yule ambaye amemruhusu kwa maandishi kwa namna ambayo Mkurugenzi ataonelea sawa.

SEHEMU YA IX
MAKOSA

47.    Kushindwa kurejeshwa tikiti zisizouzwa

    Ajenti yeyote au mtu yeyote yule ambaye ameruhusiwa na Bodi kuuza tikiti kwa niaba yake akiwa hatamrudishia Mkurugenzi au kumtumia Mkurugenzi kwa njia ya posta na kwa rejesta vishina vyote vya tikiti ambazo ameziuza au tikiti zote zisizouzwa kwa muda wa siku mbili katika tarehe ya kufunga bahati nasibu ambayo inahusiana na vishina hivyo au tikiti hizo zisizouzwa atakuwa amefanya makosa.

48.    Habari za udanganyifu

    Mtu yeyote ambaye kwa makusudi atatoa habari ya uwongo kwa Kamati ya uchunguzi ambayo imeundwa chini ya kanuni ya 40 au kwa Mkurugenzi akidai kwamba yeye au mtu mwingine ndiye mshindi wa tikiti yoyote ile iliyoshinda atakuwa amefanya makosa.

49.    Kuharibu kifurushi chenye tikiti zisizouzwa

    Mtu yeyote yule, zaidi ya Mkurugenzi au mtu mwingine aliyeruhusiwa na Mkurugenzi chini ya vifungu 43 au 44 ambaye–

    (a)    anaingia katika chumba chochote kile ambamo tikiti zisizouzwa zimehifadhiwa;

    (b)    anafungua au kujaribu kufungua sanduku ambako ndani yake tikiti zisizouzwa zimehifadhiwa;

    (c)    anafungua au kujaribu kufungua kifurushi chenye tikiti zisizouzwa ambacho kimetumwa kwa Mkurugenzi,

atakuwa amefanya makosa.

50.    Adhabu

    Mtu yeyote atakayepatikana na hatia chini ya kanuni hizi atapata adhabu ya kutozwa faini isiyozidi shilingi elfu mbili au kufungwa kwa muda usiozidi miezi miwili au adhabu zote mbili pamoja.

NYONGEZA

FOMU 1
KUTEULIWA KWA AJENTI MUUZAJI

KANUNI ZA BAHATI NASIBU YA TAIFA

(Kifungu cha 15)

Kwa:    ................................................................
................................................................
................................................................

1.    Unateuliwa kuwa Ajenti Muuzaji kuanzia tarehe .................................... katika sehemu ya 1 ..............................................................................................................................
................................................................................................................................

2.    Unaweza kuajiri wauzaji wadogo kuuza tikiti za Bahati Nasibu kwa niaba yako upendavyo katika sehemu unayoruhusiwa.

3.    Ni lazima uandike jina lako kamili na anuani yako mbele ya kila jalada la kitabu cha tikiti za Bahati Nasibu unazotumiwa, na pia unapotoa vitabu vyovyote kwa wauzaji wako wadogo hakikisha kwamba majina na anuani zao yanaandikwa katika kila kishina cha tikiti wanazouza.

4.    Wewe pamoja na Wauzaji wako wadogo hamtaruhusiwa kuuza tikiti nje ya sehemu uliyoruhusiwa.

5.    Kuteuliwa kwako kuwa Ajenti Muuzaji kutalingana na masharti kama ilivyo katika Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa, kwa masharti yafuatayo:

    (a)    kwamba utatimiza Kanuni zilizomo katika barua hii, na masharti ya Sheria za Bahati Nasibu ya Taifa, pamoja na Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa;

    (b)    kwamba kabla ya siku saba baada ya kupokea barua hii, utarudisha kwa Mkurugenzi, Bahati Nasibu ya Taifa, S.L.P. 1717, Dar-es-Salaam, vitu vifuatavyo:

        (i)    Nakala ya barua hii ikiwa imewekwa sahihi yako katika nafasi uliyowekewa; na

        (ii)    Dhamana iliyoandamanishwa na barua hii ikiwa na sahihi yako, na sahihi za wadhamini wako wawili iliowakubali, pamoja na kuwekwa stempu ya ushuru jinsi inavyotakiwa kisheria.

6.    Barua hii ya kukuteua kama Ajenti Muuzaji inaweza kuingilia kati mkataba wowote uliokubaliwa kati yako na Mkurugenzi au afisa yeyote wa Bahati Nasibu ya taifa,

    Tarehe ......................... ya leo ......................... 20........

    Nakubali kuteuliwa kwangu kuwa Ajenti Muuzaji kufuatana na Masharti na Kanuni zilizotajwa hapo juu.

Tarehe: .......................................

................................................
Ajenti Muuzaji

................................................
Sahihi ya Shahidi

    (Jina na Anuani ya Shahidi)
...........................................................
...........................................................
...........................................................

FOMU 2
HATI ZA DHAMANA

Imetolewa chini ya Kifungu 16 cha Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa, Sura 41

Kwa dhamana hii Sisi 1 .......................................................... wa ..................................
..............................................................

(hapa anayejulikana "Ajenti Muuzaji") Na 2 .......................................................................
wa ............................................................... ambaye 3 .................................................

Na 4 .......................................................... wa .............................................................
ambaye 5 .......................................................... (ambao hapa wanajulikana "Wadhamini")

tunaahidi kwa uthabiti kila mmoja wetu kwa Mkurugenzi wa Bahati Nasibu wa Taifa, Mwandani wake na kuahidi (kwa ambaye anajulikana "Mkurugenzi") kulipa kiasi cha shilingi ........................... kwa kila mchezo.

    Imewekwa Sahihi na Kutamkwa nasi Leo ......................... Mwezi ......................... 20........ Kwa kuwa Mkurugenzi amekubali kumteua Ajenti Muuzaji wa Bahati Nasibu ya Taifa, ni juu ya Ajenti Muuzaji na Wadhamini kuingia katika Dhamana ya kiasi cha fedha kilichotajwa hapo juu cha shilingi .............. kwa kila Mchezo wa Bahati Nasibu ya taifa kwa ajili ya kukubali uaminifu wa Ajenti Muuzaji na Wauzaji wake wadogo walioteuliwa na Ajenti Muuzaji kwa ahadi na mapatano ya kuteuliwa kwake kufuatana na Sheria za bahati Nasibu ya Taifa, na Kanuni za Bahati Nasibu ya Taifa; au Sheria zingine au Kanuni zitakazobadilishwa au kugeuzwa. Sasa Masharti ya Dhamana yaliyoandikwa hapo juu ni kwamba kama Ajenti Muuzaji au kila Muuzaji wake mdogo wakati akiwa bado ameteuliwa atatekeleza wajibu wake kwa Uaminifu au kama Ajenti Muuzaji na Wadhamini au mmojawapo kwa wakati wote watalipa fidia kwa Mkurugenzi kutokana na upotevu, hasara au gharama zozote zitakazogharamiwa au kuchukuliwa na Bahati Nasibu ya Taifa kutokanana na vitendo vya makosa, wizi, uongozi mbaya, uzembe kutolipa madeni au kukiuka mojawapo ya kanuni za Sheria zilizotajwa hapo juu na Ajenti Muuzaji au Muuzaji wake mdogo aliyeteuliwa na Ajenti Muuzaji hivyo kutokana na mojawapo ya mambo hayo Dhamana ambayo imeandikwa hapo juu itabadilika ama sivyo itabaki kutumika kikamilifu na kuendelea ilivyokusudiwa.

IMEWEKWA SAHIHI NA KUTAMKWA NA WATAJWAO.

.....................................................
(Ajenti Muuzaji)

.......................................................
(Sahihi ya Ajenti Muuzaji)

Na atajwaye ........................................
    (Mdhamini wa Kwanza)

.......................................................
(Sahihi ya Mdhamini wa Kwanza)

Na atajwaye .......................................
    (Mdhamini wa Pili)

.......................................................
(Sahihi ya Mdhamini wa Pili)

Mbele yangu leo ......................... Mwezi ......................... 20........

ANGALIA: Dhamana hii lazima ibandikwe stampu ya Ushuru ya shilingi ............................

{/mprestriction}